SHARE

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), kimetamba kwamba kitashinda kwa kishindo katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Monduli mkoani Arusha na Ukonga, Dar es Salaam unaotarajiwa kufanyika Jumapili ijayo.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema tathmini waliyofanya katika kampeni zinazoendelea katika majimbo hayo inaonyesha chama hicho kukubalika zaidi kwa wananchi.

“Ukonga nina imani kabisa kwamba tutashinda kwa sababu tuna uungwaji mkono mkubwa wa wananchi. Wananchi wanajitokeza kwa wingi kutuunga mkono,” alisema Dk. Mashinji na kuongeza:

“Monduli ambako watu wengi walifikiria kwamba tumelegalega na tutashindwa ndiko ambapo tumepata uungwaji mkono mkubwa zaidi kuliko hata maeneo mengine ambayo tulishawahi kushiriki uchaguzi. Rais wa mioyo ya Watanzania (Edward Lowassa) yuko huko kwa hiyo tuna uhakika kabisa kwamba kura tutapata za kutosha,” alisema.

Pia Dk. Mashinji alisema chama hicho kimejipanga zaidi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

“Mimi niwaambie Wanachadema kwamba chama kimejipanga na akili zetu tumezielekeza katika uchaguzi mkuu ujao kwa sababu ndio wenye tija kwa taifa na uchaguzi huo tutawashinda kwa kura na hatuna wasiwasi,” alisema Dk. Mashinji.

Kuhusu Baraza la Wazee la Chadema kushauri Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF), Maalim Self Sharif Hamad, kugombea urais kupitia chama hicho mwaka 2020, Dk. Mashinji alisema chama ngazi ya juu bado hawajapokea rasmi ushauri huo na kikipokea kitaufanyia kazi.

“Suala la wazee niombe tu kwamba kama chama kuna vyombo vya kufanya uamuzi. Wao kama wazee wamewakaribisha. Nina imani watakuja kuleta mapendekezo yao kwenye uongozi wa juu wa chama na tutajadili,” alisema.

“Wao ni wazee tutayasikiliza maoni yao na tutayapa uzito kulingana na watakavyowasilisha, lakini ieleweke kwamba Chadema ni taasisi na ina utaratibu wake wa kufanya makubwa kama hayo.”

Kuhusu hamahama ya wabunge na wanachama wa chama hicho, Dk. Mashinji alisema Chadema inaheshimu haki za binadamu, hivyo haiwezi kuwazuia kutekeleza haki yao ya kikatiba.

“Wengine tunaona wanaondoka saa sita usiku sasa sisi tuache shughuli zetu tukahangaike na mtu ambaye anatekeleza haki yake ya kikatiba? Chadema katika sera zetu tunasisitiza utawala bora, haki za binadamu na uhuru wa kujieleza na uhuru wa kushirikiana na watu wengine,” alisema.

“Na hata msemaji wa chama alishatoa tamko kwamba anayefikiria kwamba anataka kuondoka, aondoke salama, hatuhitaji kusuguana suguana,” alisema.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here