SHARE

SERIKALI ya Zambia wiki hii imelazimika kukanusha taarifa za kushtusha kuwa China iko mbioni kuhodhi uwanja mkubwa wa ndege wa nchi hiyo wa Kenneth Kaunda International Airport (KKIA) pamoja na Shirika la Kufua na Kusambaza umeme (Zesco) kujilipa madeni.

Hatua hiyo inachukuliwa baada ya Zambia kushindwa kutimiza masharti ya mkopo wake hivyo inalazamika kuitoa KKIA na Zesco kwa serikali ya China ili iyaendeshe mashirika hayo kibiashara na kuchukua faida kama sehemu ya kujilipa madeni.

Taarifa hizo kuihusu Zambia ziliripotiwa na jarida la Africa Confidential baada ya mkutano wa kimataifa wa China na nchi za Afrika ambapo serikali ya China ilitangaza kutoa mikopo yenye thamani ya Dola bilioni 60 kwa nchi zote 54 za Afrika.

Aidha, taarifa zilizosambaa mitandaoni zilidai kuwa kutokana na utegemezi wa mikopo ya China katika kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika nchi za Kiafrika watu wengi barani waliguswa na hayo yaliyotajwa kuendelea nchini Zambia na kuhofia kuwa yanaweza kuingia katika nchi zao baada ya Zambia.

Kwa mujibu wa Taasisi ya China Africa Research Institute iliyo chini ya Chuo Kikuu cha John Hopkins cha nchini Marekani, mikopo ya China kuelekea Afrika imekua kutoka dola bilioni tano hadi bilioni 30 kufikia mwaka 2016.

Kwa ujumla, China imekopesha nchi za Afrika Dola bilioni 136 kutoka mwaka 2000 mpaka 2017. Angola ndiyo nchi inayoongoza kwa kukopa kutoka China ambapo katika miaka 17 iliyopita wamepokea jumla ya Dola 42 bilioni.

Kupitia msemaji wake mkuu Dora Siliya Serikali ya Zambia ilisema haijashindwa kulipa madeni yake na kutaka taarifa hizo kupuuzwa.

Siliya alisema laiti kungelikuwa na hatua kama hizo, basi ni baraza la mawaziri la nchi hiyo ndilo lingelifikia uamuzi huo, na kuwahakishia raia wake kuwa hakuna kitu kama hicho.

Deni la taifa la Zambia linatazamiwa kufika Dola bilioni 13 ifikapo 2019. Takribani asilimia 30 ya deni hilo ni mkopo kutoka Uchina.

Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanaonya kuwa Zambia inaingia kwenye mtego wa madeni ya kimataifa na yaweza kupata taabu kulipa kama itaendelea kukopa kwa kasi.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here